Fasihi ni chombo na nyenzo muhimu katika kuikosoa, kuikomboa na kuielekeza jamii yoyote iwayo. Katika Afrika Mashariki, waandishi wa fasihi wameitumia sanaa hiyo pamoja na uanaharakati wao kuikosoa na kuikomboa jamii, miongoni mwa mengine. Ngugi wa Thiong’o ni miongoni mwa waandishi wanaotumia fasihi kukemea maovu katika jamii hasa utawala mbaya na kushindwa kwa serikali kutatua matatizo yanayoikabili jamii. Katika riwaya yake ya Matigari, Ngugi anakemea uporaji wa ardhi uliotekelezwa katika vipindi vya utawala wa serikali za marais Jomo Kenyatta na Daniel Arap Moi, wizi wa pesa za umma, na umaskini uliokithiri nchini Kenya. Matigari ilipigwa marufuku na serikali naye Ngugi wa Thiong’o akakimbilia uhamishoni Marekani mnamo miaka ya 1980. Waandishi wengine waliojikuta matatani kwa sababu ya maandishi na uanaharakati wao wa kisiasa ni pamoja na Abdilatif Abdallah (Kenya Twendapi?), Katama Mkangi (Walenisi), na Alamin Mazrui (Kilio cha Haki). Katika udhibiti wa kidini, riwaya ya Rosa Mistika (Euphrase Kezilahabi), kwa mfano, iliwahi kupigwa marufuku nchini Tanzania kwa madai kwamba ilikuwa ‘chafu’ na hivyo basi kupotosha maadili ya jamii. Lengo la makala haya ni kujadili mbinu na aina za udhibiti wa fasihi andishi ambazo aghalabu hutumiwa na wachapishaji na vyombo vya dola. Aidha, makala yanatathmini athari za sera ya udhibiti kwa waandishi binafsi na maoni yao kuhusu udhibiti na jinsi ya kuikwepa sera hiyo kandamizi.