Makala hii inahusu uhakiki wa Sayansi katika Tamthiliya ya Kiswahili, mifano kutoka tamthiliya ya Orodha. Ni moja ya makala chache katika mfululizo wa uchambuzi wa masuala ya kisayansi katika Tamthiliya na Fasihi ya Kiswahili kwa ujumla. Lengo la makala hii ya utafiti ni kueleza sifa fumbatwa za kisayansi zitakazopelekea kuundwa kwa mtindo mpya wa uhakiki. Mitindo ya uhalisia, uhistoria, sosiolojia, umuundo, saikolojia, falsafa, uhalisia mazingaombwe kutaja chache, imetumika kwa muda mrefu katika ulimwengu wa uhakiki. Nadharia ya mwingiliano matini imeongoza uchambuzi huu hususani kupitia usemezano wa matini. Maelezo ya ufafanuzi wa masuala ya sayansi kutoka katika taaluma za fizikia, baiolojia na kemia yalitumika kumuongoza mwandishi kuweka alama na kudondoa nukuu zilizofumbata sayansi. Data kuhusu masuala ya sayansi kutoka taaluma za sayansi kavu na taarifu ya tamthiliya zilikusanywa kupitia mbinu ya usomaji makini. Matokeo yameonesha kuwa, juhudi za kuisaka orodha au barua iliyoelezwa na mtunzi, mfasiri na wahakiki wa tamthiliya kuwa ya kuchekesha ni ya kisayansi. Wahusika Padri James, Bw. Chaka Ecko, Salimu, Juma na Kitunda wanaisaka orodha kwa kutumia mbinu ya sayansi ya utatuzi wa tatizo. Wahusika hawa wanahaha kutatua tatizo la kuipata orodha iliyoandikwa na Furaha, binti waliyetembea naye kimapenzi. Msako unatokana na hofu yao kubwa ya kutajwa kwa majina kuwa walimuambukiza ugonjwa wa UKIMWI. Mwanasayansi hufanya uchunguzi hatua kwa hatua pindi anapokabiliwa na tatizo ili kulitatua, hivyo Padri James, Bw. Chaka Ecko, Salimu, Bw. Juma na Kitunda ni wanasayansi. Sayansi hii haitajwi wazi na wahusika, mwandishi, mfasiri au wachambuzi tangulizi. Tamthiliya hii pia haikupewa sifa ya kuwa na sayansi, hadhi inayopewa na makala hii. Makala imeuweka katika ujaribizi uchambuzi wa mtindo wa usayansi kupitia mbinu ya sayansi ya utatuzi wa tatizo. Tabia hii jaribizi ya uchambuzi inasaidia wasomaji kuelewa wahusika wanavyotatua matatizo binafsi na, au jamii ambayo kwa kiasi kikubwa ni malengo ya uandishi wa kazi ya fasihi.